Psalms 18

Wimbo Wa Daudi Wa Ushindi

(2 Samweli 22:1-51)

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Mtumishi Wa Bwana Aliyomwimbia Bwana Wakati Bwana Alipomwokoa Mikononi Mwa Adui Zake Wote, Na Pia Mkononi Mwa Sauli)


1 aNakupenda wewe, Ee Bwana,
nguvu yangu.


2 b Bwana ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
Mungu wangu ni mwamba,
ambaye kwake ninakimbilia.
Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu,
ngome yangu.

3 cNinamwita Bwana anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.


4 dKamba za mauti zilinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.

5 eKamba za kuzimu zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.

6 fKatika shida yangu nalimwita Bwana,
nilimlilia Mungu wangu anisaidie.
Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika mbele zake,
masikioni mwake.


7 gDunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya milima ikatikisika,
vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika.

8 hMoshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yawakayo
yakatoka ndani mwake.

9 iAkazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.

10 jAlipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mbawa za upepo.

11 kAlifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika,
hema lake kumzunguka,
mawingu meusi ya mvua ya angani.

12 lKutokana na mwanga wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikanyesha mvua ya mawe
na umeme wa radi.

13 m Bwana alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.

14 nAliipiga mishale yake na kutawanya adui,
naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza.

15 oMabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwako, Ee Bwana,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako.


16 pAlinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.

17 qAliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.

18 rWalinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Bwana alikuwa msaada wangu.

19 sAlinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.


20 t Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.

21 uKwa maana nimezishika njia za Bwana;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.

22 vSheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.

23 wNimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.

24 x Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake.


25 yKwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia.

26 zKwa aliye mtakatifu, unajionyesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka, unajionyesha kuwa mkaidi.

27 aaWewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini huwashusha wenye kiburi.

28 abWewe, Ee Bwana, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka;
Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.

29 acKwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.


30 adKuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu,
neno la Bwana halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.

31 aeKwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Bwana?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?

32 afMungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.

33 agHuifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.

34 ahHuifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.

35 aiHunipa ngao yako ya ushindi,
nao mkono wako wa kuume hunitegemeza,
unajishusha chini ili kuniinua.

36 ajHuyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.


37 akNiliwafuatia adui zangu na nikawapata,
sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.

38 alNiliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.

39 amUlinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.

40 anUliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.

41 aoWalipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa;
walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu.

42 apNiliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo;
niliwamwaga nje kama tope barabarani.


43 aqUmeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu;
umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa,
watu ambao sikuwajua wananitumikia.

44 arMara wanisikiapo hunitii,
wageni hunyenyekea mbele yangu.

45 asWote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.


46 at Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!

47 auYeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
awatiishaye mataifa chini yangu,

48 avaniokoaye na adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.

49 awKwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee Bwana;
nitaliimbia sifa jina lako.

50 axHumpa mfalme wake ushindi mkuu,
huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.
Copyright information for SwhKC